TaTEDO yahamasisha matumizi ya jiko linalotumia joto kupikia badala ya moto kulinda mazingira.

  • Category: News
  • Published: Sunday, 13 November 2022 05:23
  • Written by Webmaster
  • Hits: 504

NA GOODLUCK HONGO

TAASISI ya Kuendeleza Huduma za Nishati Endelevu na Uhifadhi wa Mazingira Tanzania  (TaTEDO) imehamasisha matumizi ya kupikia joto badala ya moto ili kulinda mazingira na kupunguza athari za kiafya.

TaTEDO ambalo ni Shirika lisilo la kiserikali lenye malengo ya kuboresha maisha ya watanzania kwa kuchangia upatikanaji wa nishati endelevu zilizoboreshwa ,kutengeneza ajira na ongezeko la kipato ili kupambana na umasikini limekuwa likipambana kuisaidia serikali katika kufanya tafiti ili kuwa na teknolojia iliyo rafiki kwa utunzaji wa mazingira.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam Novemba 10,2022,Mkururugenzi wa TaTEDO  Estomih Sawe amesema kuwa utafiti uliofanyika unaonesha kuwa Dar es Salaam inatumia zaidi ya asilimia 60 ya mkaa wote unaozalishwa nchini ambapo miaka michache iliyopita zaidi ya tani milioni mbili za mkaa ulitumika.

“Tani Milioni moja inatumika hapa Dar es Salaam ,na hapa Dar es Salaam ni eneo ambalo karibu watu wote wana umeme,gesi na nishati zingine zote lakini bado wanatumia mkaa kwa wingi hivyo sisi tuliona umuhimu wa kuwa na teknolojia ya jiko linalotumia nishati kidogo sana ya umeme kuliko kutumia gesi,mkaa katika matumizi ya kupikia kwa haraka.

Sawe ametoa sababu zinazowafanya watu kutumia zaidi nishati ya mkaa kuwa  inatokana na mila na tamaduni ikiwemo kutokufahamu mbadala wa kutumia mkaa na kuni katika matumizi ya kupikia.

“Kwa changamoto hizo tunahitaji kuwahamasisha wananchi na kuwaelimisha ili wafahamu kwamba kuna nishati safi ambazo unaweza kutumia badala ya mkaa na ukapika chakula kwa bei nafuu,haraka na kwa usalama.

“Tunataka kuwakikishia kuwa lazima tuhamie teknolojia nyingine ya kupikia joto badala ya moto na natoa wito kwa Serikali na wananchi tushirikiane kuhusu kujua umuhimu wa kuwa na nishati mbadala katika kupikia na  upo uwezekano wa kupika kwa kutumia joto badala ya moto kwa ufanisi mkubwa na usiharibu mazingira.”amesema Sawe

Hata hivyo Sawe amefafanua kuwa ni muhimu kwa watanzania kutumia vifaa vinavyotengenezwa na teknolojia isiyoharibu mazingira kwa kuwa Tanzania itakuwa na umeme wa ziada mwingi baada ya kukamilika bwawa la Nyerere hivyo ni lazima watumie umeme huo kwa matumizi ya kupikia kupikia majiko waliyoyasanifu ambayo wanaweza kuyatumia kwa haraka na kuwahi shughuli zake zingine.

Akizungumzia kuhusu nishati safi ya kupikia,Meneja Nishati kutoka TaTEDO Mary Swai amesema wao waliamua kubuni jiko la kisasa linaloweza kupika chakula chochote ikiwemo Kande,Maharagwe,Kunde,Ugali,Nyama na vyakula vingine ambavyo hutumia gharama kubwa hadi vinapoiva kwa kutumia gharama kidogo ili kulinda mazingira na afya za watanzania.

“Hili jiko yaani Pressure cooker ni jiko,sufuria na ni nishati ya kutumika nyumbani isiyo na moshi wala kuharibu mazingira unatumia umeme kidogo kuliko ungetumia mkaa na gesi,hivyo tunawashauri wananchi wote kutumia jiko hilo la kisasa ili kupunguza gharama za matumizi ya nishati chafu kama mkaa na zingine.

“Lakini pia sisi tuna teknolojia kwa ajili ya wakulima inayoweza kukausha mazao bila kupoteza uwezo wake hivyo majiko haya ni salama kwa yeyote anayetumia kwa kuwa hujizima pindi tu muda wake uliowekwa ili kuivisha chakula hicho unapofika mwisho.

“Mfano umeweka dakika 30 ili kuivisha maharagwe au nyama au chakula kingine,pindi dakika hizo ulizoweka zikifikia basi jiko hujizima lenyewe lakini kikubwa katika jiko hilo ni kwamba linatumia sana joto katika kuivisha vyakula  badala ya moto”amesema Swai.

TaTEDO kwa kushirikiana na Mfuko wa Uhifadhi wa Mazingira Duniani (WWF) wanatekeleza mradi wa Mpito wa Nishati nchini  ambapo waliandaa warsha kwa wanahabari juu ya nishati jadidifu ikiwa na lengo la kuwaongezea uwezo juu ya nishati hiyo (Renewable Energy)katika kulinda na kuhifadhi mazingira.

Waandishi kutoka vyombo mbalimbali vya habari wengi wao kutoka Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) kikiongozwa na Mkurugenzi wake John Chikomo wameishukuru TaTEDO kwa kuandaa mafunzo hayo ambayo yamewasaidia kugundua teknolojia mbalimbali ambazo ikiwa zitatumiwa na wananchi wengi basi zitasaidia juhudi za serikali katika utunzaji wa mazingira kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.





2022 © Tatedo - Sustainable Energy Services Organization. All Rights Reserved. Designed by microsafi.com